IRINGA, SIASA, UCHUMI NA MAENDELEO
Iringa mkoa ulioko kanda ya Nyanda za juu kusini una fursa na changamoto nyingi kwa ajili ya maendeleo yake kisiasa na kiuchumi. Kwa sasa unapozungumzia Iringa unajumuisha wilaya za Mufindi, Kilolo, Iringa Vijijini na Iringa Mjini, baada ya wilaya za Rudewa, Njombe na Makete kujitoa na kuunda mkoa wake wa Njombe.
Tumefurahi kwani kuundwa kwa mkoa mpya pamoja na kuonekana kama ni kujitenga lakini ni chachu ya maendeleo. Wakati maendeleo ya Njombe yanaitegemea sana Iringa (kwa miundombinu), Iringa inaitegemea sana Njombe kwa mifumo ya Biashara hivyo kufanya mikoa hii miwili ndugu kuwa na uhusiano wa karibu na muhimu sana.
Kulingana na utafiti uliowahi kufanywa na ofisi ya Mkuu wa mkoa Iringa (ya zamani) "Per Capita GDP" ilionyesha kuwa wilaya ya Iringa kuwa na wastani mdogo wa pato huku ile ya Njombe ikiongoza. Pia ilionyesha wazi kuwa wilaya za Njombe na Mufindi zana uzalishaji wa viwanda huku Iringa Mjini ikijikita katika utoaji huduma na Kilolo na Iringa vijijini zikjikita katika Kilimo. Kwa wastani wilaya zote zilionyesha kujihusisha na kilimo isipokuwa ringa mjini kwa kiasi kidogo.
Maendeleo ya Uchumi
Tunapozungumzia maendeleo ya kiuchumi tunagusa nyanja zote zinazoendesha maisha katika mfumo wa biashara, fedha, mitaji, watu na raslimali za asili. Iringa tuna kila kitu, tuna watu, mifumo mizuri ya biashara, mitaji na raslimali asili. kinachopungua kidogo ni jinsi ya kuoanisha haya yote ili kufikia katika lengo kuu hapa nitatoa mfano.
"Wakati huduma nyingi za hotel ziko Iringa Manispaa, vivutio vingi vya utalii wa nje viko nje ya manispaa mfano Milima Udzungwa, Masalia ya Isimila, Hifadhi ya Ruaha na kwingine. Hii ni fursa pekee ambayo inaweza kuongeza mzunguko wa fedha katika maeneo yote. Jambo gumu ni kuwa, Kule RUAHA NP kuna uwanja wake wa ndege na hivyo kulazimu ndege kwenda moja kwa moja jambo ambalo linafanya huduma Mjini zisipate wateja" Huu ni mfano ambao kama ukifanyiwa kazi vizuri basi hilo linaweza kuwa si tatizo.
Iringa kuna watu, vijana wenye nguvu ya kufanya kazi; Tatizo dogo tulilo nalo ni kutokuwa na mfumo wa ujengaji ajira binafsi badala yake karibu wote tunatazama ajira za mshahara jambo linalosababisha wengi tuwe nje ya Iringa kwa sababu ya uchache wa ajira za mshahara hapo. Ipo nafasi kwa kutumia mfumo wa habari na wana habari kufanya tafiti zenye kuweka mazingira bora ya biashara halafu kuwafanya vijana wabaki mkoani kwa ajira binafsi hasa wasomi wetu.
Maendeleo ya Siasa
Hapa tuna kila sababu ya kujivunia. Kwa leo sitaeleza sana ni mafanikio gani tumeyapata kama mkoa kwa kipindi kirefu. Rai yangu kwa wana Iringa ni kuona tuna nafasi ya kuaminiwa na tuna nafasi ya kujenga nchi yetu kwa taaluma zetu na nafasi zetu. Suala la msingi ni kuwa na mfumo wenye kuwezesha urithishaji wa moyo wa utumishi bora.
Wakati ujao tutaeleza kwa urefu mafanikio makubwa tuliyopata. Blog hii inaweza kukujuza mambo mengi, kaa karibu nayo!
No comments:
Post a Comment